Na. Kitengo cha Habari na mawasiliano
Baraza la madiwani Halmashauri ya Tandahimba wameiomba serikali kupitia Wakala wa barabara vijijini na mijini (Tarura) kufanya maboresho ya barabara kwa kuzichonga hususani maeneo ya vijijini ambayo kwa sasa hayafikiki kutokana na ubovu wa miundombinu hiyo
Akielezea changamoto ya barabara Diwani wa kata ya Mihuta Hamisi Mfaume amesema kuwa miaka iliyopita barabara hizo zilikuwa zinapitika ndani ya vijiji lakini kwa sasa barabara nyingi za ndani ya Wilaya zimejifunga na kuwapa tabu wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine
“Tunawaomba Tarura walichukulie suala la barabara vijijini kama dharura hususan wakati huu wa ugonjwa wa corona (Covid – 19) barabara zimejifunga tunapata tabu kupata huduma mbalimbali ,”amesema Mfaume
Amesema awali Halmashauri ilikuwa inajitahidi kuzichonga barabara hizo na kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo lakini kwa sasa barabara hizo zimeharibika hata upitaji wa gari na pikipiki ni mgumu
“Wakati barabara hizi zipo chini ya Halmashauri zilikuwa zinapitika na zikiharibika walikuwa wajitahidi kuzichonga lakini kwa sasa Tandahimba ipo kwenye kisiwa kutokana na ubovu wa barabara ”,amesema Mfaume
Naye Mhandisi wa Tarura Wilaya Paulo Mliya akijibu hoja za madiwani amesema wanayajua maeneo yote mabovu hivyo watayashughulia mara baada ya kupata fedha
“Tunayajua maeneo ambayo hayapikiti kama vile Kata ya Mdimba na Chingungwe tutayashughulikia kwa sasa mtuvumilie,”amesema Mliya
Baraza la madiwani limefanyika jana katika ukumbi wa Halmashauri ya Tandahimba na wameweza kupitisha agenda mbalimbali sambamba na kupeana msistizo wa kuendelea kuwaelimisha wananchi katika maeneo waliyopo kuhusu ugonjwa wa Corona (Covid – 19)
TANDAHIMBA DC,MTWARA TANZANIA
Anuani ya posta: P.O.BOX 03 TANDAHIMBA
Simu: +25523 2410030
Simu:
Barua pepe: ded@tandahimbadc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Tandahimba DC. Haki zote zimehifadhiwa