●Utangulizi:
Wilaya ya Tandahimba ni moja ya Wilaya Tano zinazounda Mkoa wa Mtwara. Wilaya hii ilianzishwa rasmi Mwaka 1995.
●Mipaka wa Eneo:
Wilaya ya Tandahimba ipo Kusini mwa Tanzania. Wilaya hii inapakana na Wilaya ya Mtwara kwa Upande wa Mashariki, Magharibi inapakana na wilaya ya Newala, Kaskazini inapakana na Mkoa wa Lindi na Kusini inapakana na Mto Ruvuma ambao ni mpaka rasmi na Nchi ya Msumbiji.
Mji mkuu wa wilaya hii unaitwa TANDAHIMBA ambao upo kilometa 95 kutoka makao makuu ya mkoa wa Mtwara. Wilaya ina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 1673 sawa na hekta 167,331.
Eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 157,304 sawa na asilimia 94 ya eneo lote la wilaya, eneo lenye miti ni hekta 63,216.8 ambalo ni sawa na asilimia 38 ya eneo lote la wilaya. Misitu ya hifadhi ikiwemo hifadhi ya Milima ya Makonde ni hekta 25,218 sawa na asilimia 15 ya eneo lote la wilaya.
●Utawala.
Wilaya ya Tandahimba ina Tarafa 7, Kata 32, Vijiji 143 vilivyoandikishwa pamoja na vitongoji 654. Wilaya ina Jimbo 1 la Uchaguzi,ina miji midogo miwili Tandahimba na Mahuta
Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba ina jumla ya Waheshimiwa Madiwani 42 pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Tandahimba.
Kati ya hao,Madiwani wakuchaguliwa ni 32 na Viti Maalum ni 10. Waheshimiwa Madiwani 31 wanatoka katika Chama Tawala (CCM),Diwani 1 anatoka Chama ACT Wazalendo
●Idadi ya Watu:
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 wilaya ya Tandahimba ina watu 227,541 kati ya hao wanawake ni 122,192 na wanaume ni 105,322. Kutokana na ongezeko la watu kwa wastani wa 1.2 wilaya inakadiriwa kuwa na watu 239,947 (Ke 128,869 na Me 111,077). Wilaya ina watoto walio chini ya miaka 0 – 4 wanakadiriwa kufikia 29,842 ambao ni sawa na asilimia 13.5. Watoto umri wa miaka 5 – 19 wanakadiriwa kufikia 75,089 sawa na asilimia 33 ya watu wote wilayani, Vijana umri kuanzia 20 – 45 wanakadiriwa kufikia 72,877 sawa na asilimia 32 ya watu wote wilayani, Pia umri wa miaka 45 – 59 wanakadiriwa kufikia 26,190 sawa na asilimia 11.5 ya watu wote wilayani na Wazee umri wa miaka 60 na zaidi wanakadiriwa kufikia 23,516 sawa na asilimia 10.3 ya watu wote wilayani.
TANDAHIMBA DC,MTWARA TANZANIA
Anuani ya posta: P.O.BOX 03 TANDAHIMBA
Simu: +25523 2410030
Simu:
Barua pepe: ded@tandahimbadc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Tandahimba DC. Haki zote zimehifadhiwa